MTOTO Agnes Mtani (6), mkazi wa Kijiji cha Namarebe, Tarafa ya
Nansimo, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara amenusurika kuliwa na fisi baada
ya kuvamiwa na mnyama huyo kisha kuokolewa na wasamaria wema.
Akizungumza na Tanzania Daima jana akiwa njiani kumpeleka mtoto huyo
katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, babu wa mtoto huyo,
Mnubhi Chiremeji, alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa
12,30 jioni katika kijiji hicho.
Kwa mjibu wa Mnubhi, mtoto huyo aliondoka nyumbani kwao akiwa na dada
yake aitwaye Mariamu Mtani kwa ajili ya kwenda kuzoa udaga ulioanikwa
mwambani, mbali kidogo na nyumba yao.
Alisema wakiwa wanatembea kuelekea eneo walikokuwa wameanika udaga
huo, ghafla alitokea fisi ambaye alimnyakua mtoto huyo na kukimbia
naye.
“Baada ya dada yake kuona hivyo alipiga kelele za kuomba msaada na
kwa bahati nzuri kulikuwa na mwananchi mmoja wa kijiji hicho alikuwa
jirani, ndipo alipoanza kumfukuza fisi huyo huku pia akipiga kelele na
hatimaye alimdondosha chini, hapo ikawa pona yake,” alisema babu huyo.
Alifafanua kuwa baada ya fisi kumdondosha mtoto huyo chini, wananchi
wengine walifika na kumkuta akiwa na majeraha usoni, kichwani hadi
begani.
Aliongeza kuwa walimchukua mtoto huyo na kumpeleka katika Kituo cha
Afya Kibara na kupatiwa matibabu ya awali na baadaye kuhamishiwa kwenye
Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi.
Katika siku za hivi karibuni kumezuka wanyama aina ya fisi katika
baadhi ya vijiji vya tarafa hiyo ambao wamekuwa tishio kwa maisha ya
wananchi na mifugo.
Chanzo;Tanzania Daima
|
No comments:
Post a Comment