MWANAMKE mkazi wa
kijiji cha Ikandamoyo, wilayani Katavi, Veronica Saleh ‘Mama Kaela’ (50),
amefanya uamuzi adimu wa kuolewa na wanaume wawili ambao anaishi nao kijijini
hapo.
Kijiji hicho kipo
umbali wa takribani kilometa 30 kutoka mjini hapa katika Jimbo la Katavi
linalowakilishwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Pamoja na ndoa hiyo
iliyowezeshwa na mume mkubwa kukubali kuishi na mume mdogo, imeelezwa kuwa
mwanamke huyo ndiye ‘aliyewaoa’ wanaume hao kwa zaidi ya miaka saba sasa, huku
akiwa na amri kuu katika nyumba, kama ilivyo katika ndoa za kawaida.
Wanaume hao ni Paulo
Sabuni ‘Baba Kaela’ (60) ambaye ndiye mume mkubwa na Arcado Mlele (45) ambaye
ni mume mdogo.
Taarifa za kuwapo kwa
ndoa hiyo ya aina yake, ziliifikia Globu ya Jamii na kufanyiwa uchunguzi kwa
zaidi ya wiki tatu, na hatimaye katikati ya wiki hii, wahusika walikubali wao
wenyewe kuzungumzia suala hilo. Kwa mujibu wa maelezo ya mwanamke huyo ambaye
alionekana kuwa msemaji wa familia hiyo, yeye na mumewe mkubwa, walifika
kijijini hapo miaka 24 iliyopita, wakitoka kijiji cha Usumbwa mpakani mwa
Chunya, Mbeya na Tabora.
Wakiwa kijijini hapo
mume wake aliendelea kufanya kazi ya ukulima wakati yeye mama (Veronica),
pamoja na kilimo hujihusisha na upishi na uuzaji wa pombe ya kienyeji iitwayo
kayoga.
Mwanamke huyo ambaye
amesema ana watoto wanne, Alfred (20), binti mwenye miaka 16 (ambaye ameolewa)
na wengine wawili wa kiume, mmoja akisoma darasa la sita na mdogo ana miaka
saba, amesema hana shida na waume wake.
Ingawa wanandoa hao
walizungumza kwa hadhari, majirani walikiri kuwa mwanamke huyo anaishi na
wanaume hao wawili kwa amani na kwamba mwanamke huyo ndiye mwenye sauti na si
waume zake.
“Si siri tena sasa,
tumeshawazoea, kwani wanaishi kwa amani ila yule mume mdogo anaishi kwenye
nyumba aliyoachiwa na marehemu baba yake, lakini anashinda kwa mume mkubwa,
ambapo inajulikana kijijini hapa kuwa ni nyumba kubwa. “Basi pale ni mambo
yote, kula na kunywa, mama huyu amewapangia zamu wanaume hao kama afanyavyo
mume mwenye wake wengi.
Ama kweli ukistaajabu
ya Musa utaona ya Firauni,” alisema mkazi mmoja kwa masharti ya jina lake
kutoandikwa gazetini. Ilielezwa, kwamba wanaume hao wana akili timamu na
hawatumii kilevi cha pombe kama ilivyo kwa mke wao.
Hata hivyo, mume
mkubwa anapewa sifa za upole tofauti na mume mdogo anayetajwa kuwa mkorofi
kiasi cha mara kadhaa kumchapa makofi mkewe anapomuudhi.
Majirani wanadai
kwamba Mama Kaela na mumewe Paulo, walipofika kijijini hapo, walipokewa na
kuishi maisha ya kawaida, lakini baadaye mama huyo alianza kuwa na uhusiano wa
kimapenzi na Arcado, ambaye naye alilazimika kuachana na mkewe wa ndoa
anayefahamika kijijini hapo kwa jina la Mama Pere.
Ilielezwa na
mashuhuda hao kwamba mume mkubwa alipobaini uhusiano huo, alikuja juu, lakini
mwanamke huyo inadaiwa alimweleza mumewe huyo, atake asitake lazima wataishi
wawili, vinginevyo ataachana naye, ndipo mume mkubwa alipokubali kuishi na mume
mwenza.
Katika maisha ya
kawaida katika familia hiyo, inaelezwa kwamba katika baadhi ya siku ikitokea
kuwa mama huyo amechoka kupika, mume mdogo huchukua jukumu la kupika na
kumwandalia chakula na maji ya kuoga mume mkubwa.
“Lakini mara nyingi
kwa mfano, ikiwa ni zamu ya mama huyo kulala kwa mumewe mkubwa, basi humfulia
nguo zake kisha anakwenda kwa mumewe mdogo nako anamfulia nguo.
“Ndivyo wanavyoishi,
nasi sasa tumewazoea ila yule mama ni mkali na ana sauti pale kwake kwa wanaume
wale ila tunaona kama ana wivu sana kwa huyu mdogo ambaye naye pia ana wivu kwa
mkewe huyo, labda anahofia kuwa mama huyo anaweza kuongeza mwanamume mwingine,”
anasema mmoja wa majirani hao.
Hakuna mazuri
yasiyokuwa na machungu, japo familia hiyo inaelezwa kuwa na amani, mtoto wao
mdogo nusura avuruge uhusiano wa wanandoa hao, baada ya kuibuka mzozo wakati wa
maandalizi ya ubatizo wake.
Kwa sababu anazojua
mama, ingawa inafahamika kuwa wote ni watoto wa mume mkubwa, mke huyo katika
hati za ubatizo aliandikisha ubini wa mtoto huyo kuwa ni Mlele (akimaanisha
kuwa mtoto wa mume mdogo), lakini mume mkubwa aliweka pingamizi kanisani akidai
yeye ndiye baba halali wa mtoto huyo.
Kwa mujibu wa
mwanamke huyo, yeye na Arcado ni waumini wa madhehebu ya Katoliki wakati Paulo
ni Mpentekoste. Madai ya mzozo wa uhalali wa `ubaba’ wa mtoto huyo,
yalithibitishwa na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho, akiwamo mwalimu wa dini wa
Kigango cha Kanisa Katoliki Uruira, Mashaka Abel. Walisema miaka sita
iliyopita, mtoto huyo akiwa na umri wa mwaka mmoja, alifanyiwa taratibu za
ubatizo, lakini ilishindikana, kutokana na wanaume hao, kila mmoja kudai ndiye
baba mzazi wa mtoto.
“Lilikuwa jambo la
kustaajabisha sana, kwani familia hiyo ilifanya maandalizi yote ya sherehe ya
ubatizo wa mtoto huyo, lakini siku hiyo kanisani wakati huo ilikuwa ni kigango
cha Katumba ambacho sasa ni Uruira, sakata lilianzia pale Padri alipomwuliza
mama wa mtoto huyo ubini wa mtoto naye akasema ni Mlele.
“Hapo ndipo mume
mkubwa alipopinga na kudai kuwa mtoto yule si wa Arcado bali wake na yeye ndiye
baba halali. Padri hakuamini, aliuliza tena na tena na majibu yakawa ni yale
yale, ndipo ubatizo ukashindikana,” alisema Katekista Abel.
Kazi ya kutafuta
undani wa ndoa hiyo haikuwa rahisi kutokana na mazingira ya woga na usiri
uliokusudiwa kubaki, ambapo awali mama alisema kwamba mume wake ni Paulo pekee japo
siku ambayo mwandishi wa habari hizi alifika kijijini hapo na baadaye nyumbani
kwa wanandoa hao na kumkuta mume mdogo (Arcado akimsaidia mkewe kukoroga pombe.
Awali katika utambulisho, walidai kuwa ni mtu na mdogo wake na kusita
kuzungumzia maisha yao ya kifamilia.
Mke wao ambaye
alionekana wazi kuwa ni msemaji mkuu alifoka na kuja juu, akidai kuwa hayuko
tayari kuzungumzia uhusiano wake na wanaume hao wawili, ingawa alikiri kuwa
wanaishi pamoja.
"Kwa hiyo
umefunga safari yote hii kutoka huko ulikotoka ili uje kwangu mie Veronica …
nasema sitaki kabisa mtu kuja hapa na kutaka kunivurugia mpangilio wa maisha
yangu, kwanza nani alikueleza hayo, wambea wakubwa hao yanawahusu nini watu
hao?” alihoji.
“Mie mume wangu ni
huyu Paulo basi … sasa leo umeniachia vurugu ndani ya nyumba nitapigwa na huyo
mume wangu Paulo, kwani mmenishikisha ugoni?” alifoka Mama Kaela. Hata hivyo,
mume mkubwa alidai kuwa hatamwadhibu mkewe huyo na kwamba wataendelea kuishi
pamoja na mdogo wake Arcado kwa amani. Hata hivyo, akina mama wengi kijijini
hapo wanalaani kitendo cha mama huyo kuishi na wanaume wawili ambapo waliomba
uongozi wa Kanisa uingilie kati, ili mama huyo aweze kufunga ndoa na mume
mmoja.
No comments:
Post a Comment