Wednesday, September 21, 2016

KADHIA YA MASINONO

Ni simulizi za masaibu yaliyomkuta Baba yetu Miaka ya 70s.
Mwenyezi Mungu amlaze pahala pema peponi.
Miaka hiyo wakati akiwa Mjumbe katika Chama kikuu cha Ushirika Mara (Mara Coop) ulikuwepo utaratibu wa wajumbe kupangiwa kusimamia ununuzi wa mazao, hususani pamba kwenye vyama vya ushirika vya msingi.
Siku hiyo baada ya shughuli za mchana kutwa, usiku wa mapema soga za baraza za hapa na pale simulizi zinaelezea mianga ya tochi ilionekana kwa mbali welekeo wa magharibi, kwenye mbuga zielekezo Karukekere, mianga hiyo ilidhaniwa kuwa ya Wajaluo wakiwinda sungura. Haikuwa.......
Usiku wa manane, Chama cha ushirika cha Masinono kilivamiwa na majambazi, ilikuwa na hekaheka isiyo mfano, Kasiki la fedha lilivunjwa na fedha zilizokuwa zimebakia siku hiyo zikachukuliwa.
Wapo waliopata majeraha, Bahati njema siku hiyo Mzee CK hakudhurika.
Naikumbuka adha iliyoikumba familia yetu baada ya tukio hilo, Mzee CK na wenzie waliwekwa ndani kwa ajili ya kuwasaidia polisi katika upelelezi. Nyumbani kulipekuliwa kila pahala. Vyumbani magodoro yaliyotengenezwa kwa pamba yalichanwa, Nyasi za paa zilivurugwa vurugwa, Chooni palibomolewa na tifuatifua kila palipotiliwa shaka.
Hatukuwa na akiba yoyote pale kwetu, hivyo hakuna pesa iliyoonekana.
Baadae watuhumiwa waliachiwa kuwa huru.
Miaka mingi baadae ilikuja kujulikana, ingawa hakuna ushahidi uliokamilika kuwa kundi hili la ujambazi lilikuwa likiongozwa na mtu aliejulikana kama M......... T........... (Mungu amurehemu alipolala) ambae alifariki katika tukio la baadae kama hili la ujambazi lililoshindwa.

Baada ya takribani miaka zaidi ya arobaini tokea yalipotokea masaibu haya, nimeweza kufika Masinono. Ghala la kuhifadhia pamba la wakati huo lingalipo.

No comments:

Post a Comment