Monday, August 24, 2015

EXPEDITION TO THE GREAT WALL OF NYACHIRIGA (3)

Obhutingo bhwa Nyachiriga
Blogger kazini
Pahala lilipokuweko Boma la Nyahiti, mstali mbele ya ukuta
Juu ya Ukuta
Mapambo Magesa, Paulo (Dreva wetu) na Nyachiriga
 Bw. John Mnyaga na Bw Nyachiriga Bright
 Bw. Mapambo Magesa na Bw Nyachiriga Bright
...............tuendelee..........


...........................................Kuufikia Ukuta wa Nyachiriga ni lazima kuvivuka vilima vitatu na mabonde yenye mtandao wa mawe mengi.
Baada ya kuvuka mfereji wa maji unaotenganisha Muchigondo na kisiwa cha Kubhwenyi, mita chache kufikia “Ukuta wa Nyachiriga” tunakutana na mwenyeji wetu mwingine, huyu ni Bw. John Mnyaga. Na yeye anaanza na kuhoji ujio wetu kwenye Ukuta huu.  Baada ya maelezo ya utambulisho ya hapa na pale huku tukimsisitizia kuwa hata kwenye msafara wetu, mmojawapo ni Nyachiriga Bw. John anaridhia kutusimulia kile anachokijua kuhusu “Ukuta wa Nyachiriga”.
Bw John Mnyaga anajitambulisha kama mkazi wa Muchigondo, Mkerewe wa ukoo wa Wasilanga. Utawala wa Chifu wa Ukerewe na Mwibara. Na wao ndio wenye haki ya umiliki wa ukuta huu wa kihistoria “Obhutingo bhwa Nyachiriga”.
Ukuta wa Nyachiriga unakisiwa ulijengwa kwenye miaka inayozunguka 1840, wakati wa utawala wa Nyahiti “Omkungu”, wa ukoo wa Wasilanga watawala wa himaya ya Ukerewe na Mwibara. “Omkungu” Nyahiti alijaaliwa kuoa wanawake Kumi na mmoja (11), kati ya hao Tisa (9) walimzalia watoto wapatao Tisini (90). Hata hivyo inaelezwa kwamba watoto Sitini (60) waliuawa wakati wa mapigano mbalimbali na maadui zao. Na dhana hii ndiyo chanzo cha kuwepo ujenzi wa Ukuta huu wa mawe kwa ajili ya kukinga Boma la “Omkungu” Nyahiti ambalo lilikuwa mita chache toka ukuta huu mkuu.
Kazi ya ujenzi wa Ukuta ilifanywa na Bw. Nyachiriga, kabila Mruri wa ukoo wa Abhatandu kutoka Efulifu, maeneo ya Bhururi/Bukwaya, Musoma. Ukuta huu upatao urefu wa mita 150, na kina cha mita mbili unaanzia mita 10 ndani ya maji upande wa Magharibi na kuishia mita kumi ndani ya maji upande wa Mashariki. Ni kazi ya kipaji na ustadi wa hali ya juu ambapo mawe yamepangwa kuwa Ukuta mrefu kuzuia maadui kwa nyakati hizo kulifikia na kushambulia Boma la “Omkungu” Nyahiti.
Bw John Mnyaga (1970) anasema yeye ni kizazi cha nne cha “Omkungu” Nyahiti, hata hivyo haelewi kwa nini Ukuta huu ukajulikana kama “Obhutingo bhwa Nyachiriga” – “Ukuta wa Nyachiriga” badala ya Nyahiti ambae kwa maelezo yaliyopo ndiye Mmiliki wa Ukuta. Hakuna maelezo ya kina pia kuhusiana na hatima ya “Omkungu” Nyahiti, hata hivyo inasemekana Himaya ya Wasilanga chini ya Chifu Rukumbuzya ina uhusiano wa karibu sana na utawala wa enzi za “Omkungu” Nyahiti.
 Kwa Nyachiriga pia hakuna maelezo mengi ya kina, hata hivyo inasemekana kuna kazi nyingine mbili tatu alizozifanya za ujenzi wa kuta kama huu huko sehemu za Bhururi na Ebhwenda, Majita japokuwa hazikuwa kubwa kama Ukuta huu uliopo kisiwani Kubhwenyi. Hatima ya Nyachiriga haijulikani pia, ingawa Bw. Mapambo Magesa mkaazi wa kijiji cha Nsunsi  tuliyekutana nae katika safari yetu hii anakiri kuwa yeye ni wa Mruri wa ukoo wa abhatandu, na ana Ndugu yake mmoja anaeitwa pia Nyachiriga aliyezaliwa mnamo mwaka 1945, ambae  ni mjukuu wa Nyachiriga Mjenzi wa Kuta.
Bila ya shaka makala hii itafungua njia kwa watafiti wengine wa kihistoria wa kizazi cha leo na kijacho kwa ajili ya kupata habari zaidi za Nyahiti na Nyachiriga kwa manufaa ya vizazi vijavyo vya eneo hilo la Muchigondo, Kubhwenyi na maeneo ya jirani kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment